Rais
Jakaya Kikwete jana jioni ameongoza maziko ya sheikh mkuu wa Tanzania
Muft Issa Shaaban Simba aliyefariki jana katika hospitali ya TMJ jijini
Dar es salaam.
Maziko
hayo yalifanyika katika makaburi ya waisilamu ya nguzo nane mjini
Shinyanga na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa Shinyanga wakiongozwa na
mkuu wa mkoa huo Ally Nassoro Lufunga.
Mwili
wa marehemu uliwasili nyumbani kwake majengo majira ya saa 9 na maziko
kufanyika majira ya saa kumi baada ya ibada iliyofanyika katika msikiti
wa Ijumaa wa Majengo ambao marehemu alikuwa sheikh wake.
Wakitoa
salam za rambirambi , baadhi ya viongozi wa serikali waliohudhuria
mazishi hayo walisema hakika taifa limepoteza kiongozi imara na shupavu
ambaye alikuwa kiungo kikuu kati ya madhehebu mbalimbali ya dini na
serikali kwa ujumla.
Mbali
na Rais Kikwete viongozi wengine wa kitaifa waliopata fursa ya
kusindikiza maziko ya sheikh mkuu ni pamoja na Waziri wa mambo ya nje na
Ushirikiano wa kimataifa Bernard Membe, Mbunge wa Monduli Mh Edward
Lowassa, Waziri mkuu mstaafu Fredrick Sumaye pamoja na viongozi wengine
wa dini na serikali.
Nao
baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu mjini shinyanga walisema kifo cha
mufti Issa Simba ni pengo kubwa lisiloweza kizibika kwa haraka kwani
alikuwa kiongozi mnyenyekevu na pia alikuwa mwalimu wa kufundisha na
kuonya bila kubagua dini yoyote.
Wakati
huohuo jijini Dar es salaam makamu wa rais wa Tanzania Dk. Mohamed
Gharib Bilal jana aliwaongoza waumini wa dini ya Kiislam, viongozi
mbalimbali pamoja na watu wengine waliojitokeza katika swala ya
kumuombea marehemu Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Shaaban Issa Bin Simba
Dkt Bilal alisema taifa limempoteza kiongozi muhimu sana wa kidini na katika jamii.
Akiongea
katika swala hiyo iliyofanyika Makao Makuu ya Baraza la Waislamu
Tanzania (BAKWATA) Jijini Dar es Salaam, Dk. Bilal alimuelezea marehemu
Mufti Shaaban Issa Bin Simba kama kiongozi aliyekuwa sura ya usuluhishi
katika jamii yetu na alijenga mahusiano mazuri na serikali na katika
jamii kwa ujumla.
Naye
Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Hemed Jalala alimuelezea
marehemu Mufti Shaaban Issa Bin Simba, kuwa alikuwa ni baba wa
watanzania wote na wala hakukubali waishi kwa matabaka.
Mwili
wa Mufti Shaaban Issa Bin Simba ulisafirishwa jana asubuhi kwa ndege
kuelekea mkoani Shinyanga na maziko yake yakafanyika jioni hiyo hiyo
nyumbani kwake Majengo, Shinyanga.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.
0 comments:
Post a Comment