Pages

Ads 468x60px

Friday, June 12, 2015

Mbunge ataka taaluma ya gesi Mtwara, Lindi..........



MBUNGE wa Lindi Mjini, Salum Barwany (CUF), ametaka Serikali kutoa taaluma ya gesi na mafuta kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara.
 
Akiuliza swali bungeni jana, Barwany alisema kuna taarifa kupitia vyombo vya habari kuhusu juhudi za Serikali za kutoa taaluma ya gesi na mafuta.
 
“Je wananchi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara wananufaikaje na je ni vijana wangapi hadi sasa wamepatiwa mafunzo na wapi,” alihoji.
 
Akijibu swali hilo, Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alisema  tangu mwaka 2012/13, wizara yake imekuwa ikitoa ufadhili wa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana wa mikoa ya Lindi na Mtwara.
 
“Katika mwaka 2012/13, wizara ilifadhili wanafunzi 6o kutoka Mkoa wa Lindi na wanafunzi 50 kutoka Mkoa wa Mtwara kusomea fani mbalimbali za ufundi katika Chuo cha VETA Mtwara.
 
“Mwaka wa fedha 2013/14 wizara imefadhili   wanafunzi 59 kutoka mikoa hiyo kusomea ufundi stadi,” alisema.
 
Alisema mpaka sasa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania  (TPDC) limechangia Sh milioni 10 katika ujenzi wa maabara Mkoa wa Mtwara na Sh milioni 15 kwa ajili ya ujenzi wa maabara Mkoani Lindi na Kisiwa cha Songosongo.
 
“Mwaka 2014, Kampuni ya Ophir Energy imejenga na kukarabati shule ya msingi Lilungu iliyopo Mkoani Mtwara ambapo ujenzi umegharimu Sh milioni 600,” alisema.
 
Simachawene alisema pia kampuni za utafutaji mafuta zinawekeza katika stadi zitakazohitajika kwenye sekta ya gesi asilia kwa kujikita katika kujenga uwezo wa wakufunzi, wanafunzi na wanunuzi wa vifaa katika kusadia vyuo kutoa elimu kwa vitendo.
 
“Kwa mfano, Kampuni ya BG Tanzania inatekeleza mradi wa VETA awamu ya kwanza kuanzia Juni, 2012 mpaka 2015 kwa gharama ya Sh bilioni 2.35,” alisema.

0 comments:

Post a Comment

SHARE