BARAZA Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF), limemvua uanachama
mjumbe wake kutoka Mkoa wa Shinyanga, Chifu Lutayosa Yemba.
Chifu Yemba ambaye pia alikuwa ni mpinzani wa Profesa Ibrahim Lipumba
katika kuwania uenyekiti wa CUF kwenye uchaguzi uliofanyika mwaka jana,
alivuliwa uanachama kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za chama pamoja na
kutumia vibaya jina la mwenyekiti wa chama hicho.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho cha Baraza Kuu
kilichoanza vikao vyake jana jijini Dar es Salaam, kimesema
kuwa tuhuma za mjumbe huyo zilifikishwa mbele ya kikao hicho na
kufikiwa uamuzi huo.
“Kikao cha Baraza Kuu bado kinaendelea hapa na ajenda kubwa ilikuwa ni
tuhuma dhidi ya Chifu Yemba ambaye anadaiwa kutumia jina la Mwenyekiti
wa chama kuanzisha Saccos na hata kusababisha chama kudaiwa shilingi
milioni 12.
“Lakini pia amekuwa akitumia jina la Mwenyekiti wa chama, Profesa
Lipumba katika mradi wake huo binafsi ambao anauendesha na hata
kusababisha chama kuingia katika mgogoro hasa katika Mkoa wa Shinyanga,”
kilisema chanzo hicho.
Chifu Yemba alipambana na Profesa Lipumba katika uchaguzi wa kuwania
nafasi ya uenyekiti ambapo alipata kura 30 huku Lipumba akishinda kwa
kura 659 na kufanikiwa kukiongoza tena chama hicho.
Chanzo hicho kilisema baada ya kufikiwa kwa uamuzi wa kuvuliwa uanachama
kwa Mjumbe huyo wa Baraza Kuu, alitolewa nje ya ukumbi kwa ulinzi
maalumu hadi nje ya geti na kuondoka.
Yemba kwa muda amekuwa haelewani na hata kushambuliana katika mitandao
ya kijamii na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Abdul Kambaya ambaye
hivi karibuni alishindwa kura za maoni za kuwania ubunge wa Jimbo la
Kinondoni.
Kutokana na kushindwa huko kwa Kambaya, kuliibua hisia mbalimbali
miongoni mwa wana CUF hali iliyosababisha baadhi ya kikundi cha watu
kuandamana na kwenda Makao Makuu ya CUF kufikisha malalamiko yao kuhusu
mwenendo wa uchaguzi Kinondoni.
Alipotafutwa Naibu Mkurugenzi wa Habari wa Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya,
alithibitisha kuvuliwa uanachama kwa Chifu Yemba na kikao cha Baraza
Kuu la Uongozi la CUF.
“Ni kweli tumemfukuza uanachama mjumbe wa Baraza Kuu kutoka Shinyanga
kwa tuhuma mbalimbali, tutatoa taarifa rasmi kesho kutwa (kesho) kwa
sababu kesho (leo) tunaenda mahakamani,” alisema Kambaya.
Pamoja na kufikiwa kwa uamuzi huo, mwandishi alimtafuta Chifu Yemba
ambaye alithibitisha kufukuzwa kwake uanachama ndani ya CUF.
“Tatizo wana shaka na mimi sana, tuhuma zao zote hazina mashiko, katika
mashtaka nilikubali moja tu la kutumia nembo ya chama, ni kweli na
nikabadilisha sijaelewa jina la Profesa Lipumba nimelitumia vipi,
wamepanga kuathiri taasisi na wataniathiri kwa kweli.
“Mimi sina tatizo na CUF, naipenda katika moyo wangu lakini wao
hawanipendi na wamefanya maamuzi kikatiba, ila hizi ni hujuma za Kambaya
(Abdul) na Sakaya (Magdalena) ambao ndio walipanga kuhakikisha natoka
CUF na wamefanikiwa.
“… unajua mimi ni mwanasiasa, natafakari kwa kina hatua za kuchukua
baada ya kutokea hili. Na kwa sasa najipanga kuendelea na maisha mengine
ya kisiasa nje ya CUF,” alisema Chief Yemba.
0 comments:
Post a Comment