Hakimu wa Afrika Kusini ameamuru serikali ya nchi hiyo kumzuia Rais Omar al- Bashir wa Sudan ambaye yuko Afrika Kusini kuhudhuria Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika kuondoka nchini humo..
Jaji Hans Fabricuis amerefusha amri ya kuzuiliwa kuondoka kwa rais huyo
hadi hapo itakapotowa maamuzi ya mwisho leo Jumatatu na kuitaka serikali
kuchukuwa hatua zote muafaka kumzuia la Bashir al- Bashir asiondoke
nchini humo.
Fabricius ameagiza vituo vyote vya udhibiti wa mipaka nchini Afrika
Kusini vijulishwe juu ya amri hiyo ili kuhakikisha kwamba al- Bashir
hawezi kuondoka kabla ya kutolewa hukumu.
Al- Bashir ameonekana akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine
wa Kiafrika katika mkutano huo wa kilele mjini Johannesburg Jumapili
(14.06.2015) akiwa ndani ya suti ya rangi ya bluu na kutabasamu wakati
wakipigwa picha.
Bashir Awekewa Kinga:
Chama cha ANC ambacho ndio chama tawala nchini humo kimesema serikali
ya Afrika Kusini imewawekea kinga ya kutokamatwa washiriki wote wa
mkutano huo wa kilele ikiwa kama ni kanuni ya kimataifa kwa nchi zenye
kuandaa mikutano hiyo ya Umoja wa Afrika au hata Umoja wa Mataifa.
Chama hicho kimesema kwamba kwa msingi huo miongoni mwa mambo mengine
ANC inaitaka serikali kupinga amri hiyo inayoilazimisha serikali ya
Afrika Kusini kumkamata Rais al Bashir na kuongeza kusema kwamba nchi za
Kiafrika na Ulaya ya Mashariki zinaendelea kubebeshwa maamuzi ya
mahakama hiyo ya ICC pasipo haki.
Hata kabla ya mkutano huo wa Jumapili Umoja wa Afrika ulikuwa umeitaka
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kusitisha mchakato wa kesi zake dhidi
ya marais wanaokuwa madarakani na kusema kwamba haitolazimisha nchi
yoyote mwanachama kumkamata kiongozi kwa niaba ya mahakama hiyo.
Al- Bashir amekuwa akisafiri nchi za nje hapo kabla na hakuna serikali
ya kitaifa iliomkamata kwa niaba ya mahakama ya ICC yenye makao yake
mjini The Hague, Uholanzi.
Wajibu wa kisheria
Kituo cha Haki za Kisheria cha Kusini mwa Afrika ambacho ni
shirika la haki za binaadamu kimesema kimepata hukumu ya jaji yenye
kuilazimisha serikali kumzuia al Bashir kuondoka Afrika Kusini wakati
mahakama ikisikiliza hoja za kutaka akamatwe kwa madai ya mauaji ya
kimbari na vitendo vyengine vya kihalifu.
Mwendesha mashtaka wa Mahakama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu Fatou
Bensouda amesema Afrika Kusini ina wajibu wa kisheria kumkamata na
kumsalimisha al Bashir kwa mahakama hiyo ya ICC.Ofisi yake imekuwa
katika mawasiliano na serikali ya Afrika Kusini kuhusiana na ziara hiyo
ya rais wa Sudan.
Iwapo al- Bashir hatokamatwa suala hilo litafikishwa kwa baraza la nchi
wanachama wa mahakama hiyo na kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
ambalo ndio lililofikisha kesi ya jimbo la Dafur nchini Sudan kwa
mahakama ya ICC hapo mwaka 2005.
Mzozo wa Dafur
Mashtaka dhidi ya al- Bashir ambaye ameingia madarakani katika
mapinduzi ya mwaka 1989 yanatokana na unyama ulioripotiwa katika mzozo
wa Dafur ambapo watu 200,000 wameuwawa na wengine milioni mbili
wamepotezewa makaazi yao kutokana na mashambulizi ya serikali.
Rais huyo wa Sudan tayari ametembelea Malawi,Kenya, Chad na Congo miaka
michache iliyopita nchi ambazo zote ni wanachama wa mahakama ya
ICC.Mahakama hiyo haina nguvu yoyote ile ya kuzilazimisha nchi kumkamata
kiongozi huyo na inaweza tu kuzieleza kwamba zina wajibu wa kisheria
kufanya hivyo.
Sudan imesisitiza kwamba ziara ya rais wao nchini Afrika Kusini
inaendelea vyema na atarudi nyumbani baada ya kumalizika kwa mkutano huo
wa kilele wa Umoja wa Afrika.
0 comments:
Post a Comment