Wanawake
nchini wametakiwa kuacha kutumia rushwa ya ngono ili waweze kuchaguliwa
katika nafasi mbalimbali za uongozi bali watumie uwezo wao kupambana
ili waweze kushika nafasi za juu kwenye ngazi za maamuzi.
Hayo
yalibainishwa na aliyekuwa mbuge wa Ukerewe (CCM), Balozi Getruda
Mongela (pichani), wakati alipokuwa akifungua kongamano la kitaifa la
wanawake mjini Dodoma.
Alisema mwanamke anayetumia ngono ili aweze kuchaguliwa katika uchaguzi hafai kuongoza na jamii haina budi kumwogopa.
“Mwanamke
ambaye anatumia rushwa ya ngono ili kupata uongozi huyo ni mwasherati
na hapaswi kuaminiwa katika kupewa nafasi yeyote ya madaraka katika
serikali yoyote ile,” alisema Mongela.
Aidha,
alisema kuwa katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka
huu wanawake wanatakiwa kuwa kitu kimoja bila kujali itikadi zao za
vyama kwani wao ndiyo wamekuwa wakipata shida katika kutafuta huduma
mbalimbali za kijamii.
“Mimi
nikiwa Chadema na wewe CCM lakini mwisho wa siku tunakutana hospitali
ili kuweza kujifungua tukiwa wodi moja hivyo basi sisi tuwe na ajenda
yetu moja kama wanawake,” alisema.
Alisema
kuwa pia wanawake wanatakiwa kuachana na imani za kishirikina katika
uchaguzi ujao kwa kuwa haiwezi kuwasaidia hata kidogo kuingia madarakani
bali wawe karibu na wananchi na kupanga sera zao zenye tija.
“Kama
uchawi ungekuwa unauwezo huo basi wale waganga wa kienyeji wao kwanza
wangekuwa wabunge unafikiri kwani wao hawapendi kuwa wabunge?” alihoji.
Hata
hivyo, aliwataka wanawake kuwa na tabia ya kuthubutu katika kufanya
maamuzi yao na kuweka uwoga pembeni kwa kuwa hiyo ndiyo itakuwa silaha
yao katika kupata nafasi za juu za uongozi.
0 comments:
Post a Comment