HATIMAYE Serikali imekubali kuuondoa bungeni Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa mwaka 2015.
Muswada huo, ambao unapingwa na wadau wa habari, ulikuwa usomwe leo bungeni kwa mara ya pili na tatu.
Akitangaza
kuondolewa kwa Muswada huo bungeni jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, alisema Serikali imetafakari na
kuyakubali maoni ya Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii ya kutaka
kuendelea kuufanyia kazi muswada huo.
“Serikali
imeafiki muswada huo uendelee kufanyiwa kazi hadi hapo Kamati
itakapokuwa imekamilisha kazi yake ipasavyo na kuwasilisha maoni yake
bungeni,” alisema.
Profesa Mwandosya alisema matarajio ni kwamba muswada huo utasomwa kwa mara ya pili na ya tatu katika Bunge lijalo.
“Muswada
wa Sheria ya Upatikanaji Habari wa mwaka 2015, ulichapishwa Februari
20, mwaka 2015 na ukasomwa kwa mara ya kwanza bungeni katika Mkutano wa
19, kwa hiyo muswada huu si wa dharura kama wengine wanavyosema,” alisema
Alisema
hata hivyo, Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii iliyokutana Juni 22
mwaka huu iliujadili kwa kina na kuzingatia maoni ya wadau wa tasnia
hiyo muhimu ikashauri kupewa muda zaidi kwa ajili kuendelea kupata maoni
zaidi ya wadau.
“Naomba
kutoa ushauri kwa wadau ambao bado wanaendelea kutoa maoni kwa Kamati
na wale ambao hawajatoa ushauri waendelee kufanya hivyo ili kupata
Muswada ulio bora na sheria nzuri kwa maslahi ya Taifa,” alisema.
Profesa
Mwandosya alisema mchakato wa kutunga sheria za nchi ni shirikishi na
ni wa wazi na kwamba sheria inayokusudiwa kutungwa kila wakati huwa ni
kwa manufaa ya jamii na kwa Taifa.
Wadau
mbalimbali wa habari wamekuwa wakipinga kuwasilishwa kwa muswada huo
bungeni kwa sasa kutokana na kutokukidhi viwango na kutozingatia maoni
ya wadau.
Baadhi
ya wadau hao ni pamoja na Jukwaa la Wahariri (TEF), Chama cha Wamiliki
wa Vyombo vya Habari (MOAT), Baraza la Habari la Nchi za Kusini mwa
Afrika tawi la Tanzania (MISATAN), Mtandao wa Watetezi wa Haki za
Binadamu na Jukwaa la Katiba na baadhi ya asasi zisizo za kiraia.
0 comments:
Post a Comment