CHAMA
cha ACT- Wazalendo kimesema kitaleta sera mahususi na zenye mapinduzi
kuhusu utajiri wa nchi unavyopaswa kuwa na faida kwa wananchi wake.
Hayo
yalisemwa na Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe, alipokuwa akihutubia
katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Nkanaredi,
mkoani Mtwara.
“Tuna
utajiri wa madini, mafuta na gesi. Hapa Mtwara ni kituo kiongozi cha
harakati za wananchi kufaidi maliasili zao. Mliumizwa katika harakati
hizo muhimu sana za kuhakikisha kuwa utajiri wa nchi unatumika kwa ajili
ya wananchi,” alisema.
Alisema
Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imetangaza miswada ya sheria ya
kurekebisha sekta ya mafuta na gesi, ambapo wamepeleka miswada hiyo
bungeni kwa ajili ya kujadiliwa, huku ikiwa haijawahusisha wananchi.
“Miswada
hii ni miswada muhimu sana kuhusu namna utajiri wa mafuta na gesi ya
nchi yetu unapaswa kusimamiwa. Serikali imepeleka miswada hii chini ya
hati ya dharura. Kama kuna wadau wakubwa katika sekta ya mafuta na gesi
hakuna wadau zaidi ya watu wa Mtwara na Lindi.
“Miswada
hii inapelekwa bungeni bila kupata maoni yenu. Haikubaliki, ACT
Wazalendo inataka miswada hii iondolewe bungeni ije kwa wananchi ipate
maoni na kujadiliwa na Bunge la 11 litakalopatikana baada ya uchaguzi
mwaka 2015.
“Muswada
wa Mafuta umetungwa bila ya kuzingatia mchakato wa Katiba ya nchi.
Rasimu ya Katiba imeondoa suala la mafuta na gesi kwenye orodha ya mambo
ya Muungano. Sheria iliyopelekwa bungeni inatamka kuwa sheria hiyo
itatumika Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar,” alisema.
Zitto
alisema muswada wa usimamizi wa mapato ya mafuta na gesi pia umetamka
kutumika pande zote za Muungano kinyume na nia ya kuondoa masuala ya
mafuta na gesi katika orodha ya mambo ya Muungano.
“Ni
kichekesho na Serikali kuahidi kwa Wazanzibari kuwa mafuta na gesi si
suala la Muungano halafu inatunga sheria za mafuta na gesi za kutumika
Zanzibar. Miswada hii haikufikiriwa vizuri na hivyo iondolewe."
Alisema
muswada wa mapato ya mafuta na gesi imeandikwa haraka haraka na umeacha
kabisa kushughulikia suala la mgawo wa mapato ya mrabaha kwa maeneo
yenye utajiri huo.
0 comments:
Post a Comment