Pages

Ads 468x60px

Friday, June 19, 2015

‘Wanaowatia Mimba Watoto Watungiwe sheria Kali’



SERIKALI imetakiwa kupunguza tatizo la kuwatia watoto wadogo mimba kwa kutunga sheria kali zitakazochukuliwa dhidi ya watakaobainika kufanya vitendo hivyo.
 
Kauli hiyo imetolewa jana na Diwani wa Kata ya Mnadani, Steven Masangia, katika kilele cha Siku ya Mtoto wa Afrika ambapo kiwilaya ilifanyika Shule ya Sekondari Kikuyu B na kazi hiyo ilikwenda sambamba na watoto kupewa matone ya Vitamin A pamoja na dawa za minyoo.
 
“Serikali ina jukumu la kutunga sheria kali kwa wale wanaowatia watoto mimba kwani wamekuwa wakiwafanya washindwe kuendelea na masomo pamoja na kuwaharibia maisha yao ya baadaye,” alisema Masangia.
 
Masangia alisema ili kuwakinga watoto na janga hilo, ni muhimu kwao kukataa kukubali ofa wanazopewa za chipsi na zawadi ndogondogo kwa kuwa zimekuwa kichocheo cha kurubuniwa.
 
Diwani huyo alitoa wito kwa mashirika ya dini kulikemea jambo hilo kwa nguvu zote kwa kuwa halimpendezi hata Mungu.
 
“Niwaombe watoto mliopo hapa msikubali zawadi ndogondogo na chipsi kwani zimekuwa chanzo cha kutiwa mimba katika umri mdogo.
 
“Wazazi wana jukumu la kuhakikisha wanawapa elimu watoto hasa wale wenye ulemavu kwa kuweka miundombinu ambayo ni salama kwao,” alisema.
 
Masangia alitumia hotuba yake kukemea mauaji ya albino ambao alisema nao wana haki ya kuishi kama walivyo wengine.
 
Kwa upande wa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kikuyu B, Tatu Mohammed, aliitaka jamii kushirikiana ili kutokomeza tatizo la mimba za utotoni kwani kwa kufanya hivyo watapunguza magonjwa kama vistula.
 
Alisema tatizo lingine wanalokabiliana nalo ni watoto kuolewa katika umri mdogo hali inayochangia kupata magonjwa mengi kutokana na kutokomaa kwa nyonga.

0 comments:

Post a Comment

SHARE