Chama
cha Wananchi (CUF), kimeibuka na kumtetea aliyekuwa Mbunge wa Monduli,
Edward Lowassa (pichani juu), kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM),
kilimuonea kwa kukata jina katika ngazi ya Kamati ya Maadili na
kushindwa kulifikisha Kamati Kuu ya CCM (CC).
Lowassa
alikatwa jina lake akiwa ni miongoni mwa wagombea 38 wa urais kupitia
CCM, lakini inadaiwa kwamba aliondolewa katika hatua za awali kwenye
Kamati ya Maadili.
Kadhalika,
CUF kimesema kipo tayari kumpokea Lowassa ndani ya chama hicho kwa kuwa
ni msafi na hajawahi kufikishwa hata mahakamani kwa ajili ya
kushitakiwa kutokana na madai ya rushwa.
Kauli
hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa
CUF, Abdul Kambaya, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha
Pilikapilika za uchaguzi nchini kinachorushwa na kituo cha Televisheni
cha Star Tv.
Kambaya
alirejea ripoti ya Kamati teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harrison
Mwakyembe mwaka 2008 kuchunguza kashfa ya Richmond ambayo ilimng'oa
Lowassa katika nafasi ya Waziri Mkuu.
Alisema
katika kamati hiyo, Dk. Mwakyembe aliweka bayana kwamba kila mtu
aliyehusishwa ama kutajwa katika kashfa ya Richmond angefikishwa
mahakamani kujibu mashtaka.
Kambaya
alisema mpaka sasa Lowassa hajawahi kufikishwa mahali popote
kushitakiwa na kwamba hatua hiyo inaoonyesha kwamba kiongozi huyo hakuwa
na kashfa yoyote.
Alisema
lengo la CUF ni kuing'oa CCM na kwamba ukiona kuna mtu mwenye uwezo
mkubwa wa kuitikisa chama hicho na kukipasua wapo tayari kumkaribisha
ili washirikiane naye.
Alifafanua
kuwa mtu ambaye siyo msafi hawezi kukaribishwa CUF na kwamba Lowassa
kama angekuwa mchafu angekuwa ameshitakiwa mahakamani tangu alipojiuzuru
mwaka 2008. Katika mjadala huo washirki walijadili matumizi makubwa ya
fedha yaliyojionyesha ndani ya CCM tangu mchakato wa kuelekea Uchaguzi
Mkuu ulipoanza.
Watu
wengine waliojitokeza kumtetea Lowassa ni pamoja mwanachama mwenye kadi
namba nane ya CCM, Kingunge Ngombale Mwiru, ambaye alitamka wazi kwamba
kanuni na sheria ndani ya chama zilikiukwa.
Kingunge
alisema haki haikutendeka kwa sababu Kamati ya Maadili kwa mujibu wa
kanuni na taratibu za CCM haina mamlaka ya kukata jina la mgombea kwa
sababu siyo kikao cha maamuzi. Wakati hayo yakisemwa, Katibu wa Itikadi
na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amewaonya watu wanaokisema vibaya chama
hicho na kwamba kitawachukulia hatua.
0 comments:
Post a Comment