NAIBU
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, amesema
kwa sasa nchi ipo njia panda, hivyo kuna haja ya kutumia busara ili
kuchagua kiongozi atakayeleta maendeleo.
Kauli
hiyo aliitoa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki , wakati akizungumza na
wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Tawi la Mwenge, kuhusu utandawazi na
maendeleo ya jamii.
January,
Mbunge wa Bumbuli, ambaye pia ametangaza kutaka kugombea urais, alisema
Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu ni muhimu kuliko zote,
kutokana na wananchi kuwa njia panda ambayo moja ina mashimo na nyingine
ina mafanikio.
Alisema
matamko mbalimbali ya viongozi wa dini katika sherehe za sikukuu na
mwaka mpya yanaonyesha nchi ipo njia panda kutokana na wananchi kukosa
amani ya moyo.
“Uchaguzi
huu una majaribu mengi, kuna viongozi wanafanya kazi ya kutoleana lugha
kali na kushutumiana wizi, tafadhali angalieni uchaguzi huu ni muhimu
na tunaweza tukachagua watu watakatuingiza shimoni ama watakaoweza
kutupeleka katika mafanikio,” alisema January.
Alisema
hiki ni kipindi cha tatu ambacho Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaingia
katika uchaguzi wa ndani, hivyo anaamini bado kinaendelea kujifunza
katika masuala hayo.
Alisema
kuna mambo yanaonyesha wazi kuwa katika kipindi hiki nchi inajaribiwa,
hivyo busara za viongozi zinahitajika ili kuweza kuivusha nchi salama
na watu waishi vizuri baada ya uchaguzi.
Alisema
vijana pia wana nafasi kubwa ya kupaza sauti ili kupata viongozi bora,
ikiwa pamoja na kuuliza maswali kuhusu hatima ya nchi badala ya
kushabikia.
Mmoja
wa wanafunzi alimuuliza endapo atakuwa rais atafanya nini ili Ikulu
isiwe pango la walanguzi, lakini alijibu hawezi kuongelea masuala ya
siasa katika eneo la taaluma.
“Nisingependa
katika mazungumzo haya kusema nitafanya nini nikichaguliwa ili
mnichague, swali linaloelekeza huko sitojibu, tusifanye siasa kwa sababu
hii ni sehemu ya taaluma, kama unataka mambo hayo nitafute mtaani au
katika mitandao,” alisema January.
Pia
aliitaka Tume ya Uchaguzi (NEC) kuharakisha mchakato wa uandikishaji
wapiga kura ili kuhakikisha watu wanapata haki ya kupiga kura.
Alisema
hatafurahi kuona mtu anashindwa kupiga kura kwa sababu za
kutojiandikisha, badala yake asiyepiga kura awe ni kwa sababu zake
binafsi.
0 comments:
Post a Comment