SERIKALI
imewaomba wananchi kushirikiana na taasisi za Serikali pamoja na
mashirika binafsi, kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu
ulioibuliwa na wakimbizi kutoka nchi jirani ya Burundi.
Wito
huo umetolewa jijini Dar es Salaam juzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Donald Mbando, wakati akifunga mkutano wa
tatu wa sayansi ya afya ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi
Shirikishi Muhimbili (Muhas).
Alisema
kutokana na wimbi la wakimbizi wa Burundi walioingia mikoa ya Kigoma na
Kagera, kumesababisha magonjwa ya mlipuko yakiwamo kipindupindu ambao
ni hatari iwapo hakutakuwapo na ushirikiano wa kutosha kudhibiti ugonjwa
huo ambao mpaka sasa umesababisha vifo vya wakimbizi saba.
Aidha,
aliwataka watafiti wa masuala ya afya nchini kuhakikisha kwamba
wanaibua hoja mpya kuhusiana na masuala ya afya zitakazosaidia kuleta
mabadiliko kwenye sera za taifa zinazohusu masuala ya afya.
“Kwa
sasa taifa linashuhudia ongezeko kubwa la idadi ya watu wanaosumbuliwa
na magonjwa yasiyo yakuambukizwa kama vile kisukari na shinikizo la
damu. Kwa bahati mbaya vituo vyetu vingi vya afya havijaandaliwa vizuri
kukabiliana na magonjwa haya kwa sababu sera zetu wakati zinaandaliwa
hazikujikita zaidi kwenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza ndio maana
tunahitaji mabadiliko kwenye hili,” alisema Dk. Mbando.
Dk.
Mbando alizataja sababu kubwa zinazochangia ongezeko la magonjwa hayo
kuwa ni pamoja na matumizi ya pombe kupita kiasi, aina ya vyakula
vinavyotumiwa na Watanzania hususani wale wanaoishi maeneo ya mijini,
kutokufanya mazoezi pamoja na uvutaji wa sigara.
Aliongeza
kuwa kwa sasa Serikali ipo kwenye mpango wa kuandaa mkakati wa nne wa
huduma za afya hapa nchini utakaomwezesha kila Mtanzania kuwa na bima ya
afya.
“Kwa
sasa ni asilimia 20 tu ya Watanzania ndio wanamiliki bima za afya
zinazotolewa na Shirika la Bima ya Afya la Taifa na mashirika binafsi na
hivyo kufanya asilimia 80 ya Watanzania kuishi bila kuwa na uhakika wa
masuala ya tiba….hili tumelianza tayari,” alibainisha.
Akizungumza
kwenye mkutano huo, Makamu Mkuu wa Muhas, Prof. Ephata Kaaya, alisema
kwa sasa taifa linahitaji zaidi tafiti za kiafya hususani kwenye
magonjwa yasiyo ya kuambukiza na ndio sababu mkutano huo ulijikita zaidi
kujadili tatizo hilo.
Mkutano
huo wa siku mbili ulihudhuriwa na washiriki zaidi ya 300 wakiwemo
madaktari, viongozi na wanafunzi wa udaktari kutoka Muhas na vyuo
vingine vya afya.
0 comments:
Post a Comment