SERIKALI imekiri kuruhusu uanzishwaji wa kiwanda cha kusindika nyama ya punda kilichopo hapa nchini.
Imekiri
hivyo baada ya Mbunge wa Ole, Rajab Mbarouk Mohamed (CUF), kuibua hoja
hiyo juzi jioni wakati wa kupitisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Katika
hoja yake, alitaka kujua juhudi zilizofanywa na Mamlaka ya Chakula,
Dawa na Vipodozi (TFDA), kukagua viwanda vya usindikaji wa chakula ikiwa
ni pamoja na kiwanda hicho.
Aliilaumu
Serikali kukaa kimya bila kutoa taarifa za kiwanda hicho ambacho
mwekezaji wake ni raia wa kigeni kutoka China, huku akihoji iwapo nyama
hiyo ni salama kwa matumizi ya binadamu.
Alisema
uzalishaji wa nyama hiyo licha ya kuashiria kutoweka kwa wanyama kazi
hao, lakini pia unaweza kuzua hofu ya kiimani miongoni mwa jamii
kutokana na nyama hiyo kuingizwa sokoni.
“Nataka kujua usalama wa vyakula vinavyosindikwa katika viwanda mbalimbali je, TFDA inatumia njia gani kuhakiki hivi viwanda?
“Ripoti
ya Shirika la Afya Duniani (WHO), inasema aina ya maradhi zaidi ya 200
duniani yanasababishwa na ulaji wa chakula kisicho salama.
“Sasa
hivi kuna kiwanda hapa nchini kinachakata nyama ya punda, ipo hatari ya
hawa punda virongwe (wanyama kazi) kuadimika kwa kuwafanya kitoweo,” alisema Rajab.
Hata hivyo, aliishangaa Serikali kuruhusu kiwanda hicho bila kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na matumizi ya nyama hiyo.
“Mimi
napata wasiwasi mkubwa kuhusiana na nyama hii, kwanza uzao wa punda ni
mdogo, sasa kuwavuna kwa ajili ya kitoweo kunatishia wanyama hawa
kutoweka.
“Lakini
hata hivyo mimi nashangaa, hapa Tanzania tunao ng’ombe wengi, mbuzi,
kondoo na kuku wa kutosha tumeshindwa kuwekeza katika mifugo hii halali
hadi tuanze kuchinja punda ndiyo uwekezaji uliofika huo?” alihoji.
Akijibu
hoja hiyo, Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk. Titas Kamani,
alikiri uwepo wa kiwanda hicho na kusema kuwa nyama hiyo imepimwa na
wataalamu na haina madhara kwa binadamu.
Alisema nyama ya punda inayozalishwa katika kiwanda hicho inasafirishwa nje ya nchi na haitumiki kwa mahitaji ya soko la ndani.
“Hapa
kati kati kulikuwa na wimbi kubwa la wanyama kazi hawa kusafirishwa
kwenda Kenya huko kuna viwanda hivi, sasa tulioana bora tuwachinje na
kuwasindika wenyewe kisha tuuze nyama tupate fedha,” alisema Dk. Kamani.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen
Kebwe, alisema wizara yake kupitia TFDA imefanya uchunguzi na
kujiridhisha kuhusiana na ubora wa nyama hiyo.
0 comments:
Post a Comment