MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema amesema uandikishaji wapigakura
katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, uliokuwa uanze jana na
kuahirishwa, umewasikitisha kama chama kwa kuwa wananchi hawakupewa
taarifa za usitishwaji wa uandikishaji huo.
Licha ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoa taarifa kwa vyombo vya
habari kuhusu kusitishwa huko, wananchi walijitokeza jana kwenye vituo
vyao kwa ajili ya kujiandikisha.
Lema alisema hayo jana jijini Arusha wakati alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari na kulalamika kuwa wananchi hawajaelezwa sababu ya
kuahirishwa kwa uandikishaji huo, ambao awali ulikuwa ufanyike Juni 12
na kutangazwa tena kuwa utafanyika Juni 9 na juzi NEC ilitangaza kuwa
utafanyika Juni 15 mwaka huu.
Alisema NEC wameahirishwa bila kutoa taarifa kwa viongozi wa vyama
mbalimbali vya siasa, ambao walijipanga vyema kuhakikisha zoezi hilo
linafanyika na wananchi wanajiandikisha ili waweze kuwa na vitambulisho
hivyo kwa ajili ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
“Kuahirishwa kwa zoezi hili ni hujuma zinazofanywa na NEC, maana
wametangaza kuahirisha zoezi wakati wananchi leo walikuwa wamejitokeza
katika vituo vilivyopangwa kuanza zoezi hili la uandikishaji, lakini
tunasema hizi ni hujuma za makusudi za kuhakikisha wannachi
hawaandikishwi, lakini na sisi tunasema tutaendelea na uhamasishaji wa
kuajiandikisha kwa wananchi ili tarehe hiyo nyingine wajitokeze kwa
wingi.
"Pia, ingawa kuna ongezeko la idadi ya kata za jiji hilo, ongezeko
hilo si kigezo cha kuahirisha uandikishwaji, lakini na sisi tutaendelea
na kampeni zetu za kata kwa kata, kuhamasisha uandikishaji hadi zoezi
hilo litakapoanza la uandikishwaji kwa mfumo wa BVR."
Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Arusha, Richard Kitwega aliomba radhi kwa
wananchi wa Mkoa wa Arusha, kutokana na tume kusitisha zoezi hilo na
kutaja sababu zilizofanya uandikishwaji huo kutofanyika jana kuwa ni
ongezeko la kata, vifaa vya kuandikisha kutokamilika ikiwemo wino na
kuahidi kuwa zoezi hilo litafanyika Juni 15 mwaka huu.
Awali, juzi Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Idd alisema zoezi hilo
lilitakiwa kuanza jana kwa kata sita na baada ya siku saba zoezi hilo
litaendelea katika kata nyingine za jiji la Arusha.
0 comments:
Post a Comment