MJUMBE
wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Taifa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida,
Jonathan Njau, ametangaza kugombea kwa mara nyingine nafasi ya ubunge
katika Jimbo la Singida Mashariki, baada ya mwaka 2010 kushindwa
kufurukuta kwa Mbunge wa jimbo hilo, Tundu Lissu.
Katika uchaguzi huo wa mwaka 2010, Njau alishindwa kwa tofauti ya kura 1,626.
Mwanasheria huyo mkongwe, aliyasema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na mamia ya wana CCM.
Alidai kuwa safari hii amejipanga vizuri zaidi kushinda kwa kishindo nafasi hiyo.
Alisema
ameamua kupeperusha tena bendera ya CCM kwenye kinyang’anyiro hicho
baada ya kubaini kwamba kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, jimbo
hilo limerudi nyuma kimaendeleo.
“Ndugu
zangu wa Jimbo la Singida Mashariki, kila mmoja wenu ni shuhuda mzuri
kwamba kuanzia Oktoba mwaka 2010 hadi sasa, jimbo letu limekuwa nyuma
mno kimaendeleo katika sekta zote. Maendeleo pekee yaliyopatikana ni
wananchi kuendelea kupotoshwa wasichangie wala kushiriki utekelezaji wa
miradi yao ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa maabara,” alisema Njau ambaye hata baada ya kupinga matokeo hayo yaliyomwingiza madarakani Lissu alishindwa.
Akifafanua,
Njau alisema wapotoshaji hao wakubwa kama wangekuwa wana mapenzi ya
dhati na Jimbo la Singida Mashariki, wangekuwa hata na nyumba ya kuishi
jimboni na sio kutegemea nyumba za kulala wageni.
“Nawaombeni
wana CCM wenzangu na wananchi wa Jimbo la Singida Mashariki,
tuunganishe nguvu zetu pamoja ili Oktoba mwaka huu mnipe kura za
kutosha, ili sote tushirikiane kuliendeleza jimbo letu kwa manufaa ya
kizazi cha sasa na kile kijacho,” alisema Njau.
Kuhusu
zoezi la uandikishaji kwenye daftari la wapiga kura, Njau amewataka
wananchi wote wahakikishe wanajiandikisha ili kujijengea mazingira
mazuri ya kuchaguliwa na kuchagua viongozi bora kwenye uchaguzi mkuu.
“Mimi
niwaombe tu ndugu zangu na hasa vijana, tuepukane na tabia ya kufuata
mkumbo, kila mmoja wetu afanye maamuzi sahihi na sio maamuzi
yanayotokana na kushawishiwa. Chagueni kiongozi ambaye hatatumia hila,
ulaghai, upotoshaji na rushwa katika kujipatia kura, mkikubali
kupotoshwa basi jimbo hili litaendelea kuwa la mwisho kimaendeleo kati
ya majimbo yote hapa nchini,” alisema Njau.
0 comments:
Post a Comment