MILIO ya risasi ilisikika katika vituo vya uandikishaji kura katika
kata ya Sokoni One jijini hapa, baada ya kuibuka kwa vurugu
zilizohusisha vijana wa Chadema na wenzao wa CCM, chanzo kikitajwa madai
ya kuwepo kwa watu ambao sio wakazi wa eneo hilo kutaka kujiandikisha.
Vurugu hizo zilisababisha takribani watu 15 kukamatwa akiwemo Mbunge
wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) ambaye hata hivyo
baadaye aliachiwa huru. Alishikiliwa kuanzia saa 1:30 usiku hadi saa
4:00 usiku juzi.
Patashika hiyo ilichukua zaidi ya saa moja, kwani baadhi ya polisi
waliokuwa na silaha za moto aina ya bastola walifyatua risasi hewani kwa
lengo la kutawanya vurugu hizo, lakini hali ilikuwa mbaya zaidi hadi
polisi walipoongezwa na kufanikiwa kutuliza ghasia hizo.
Wakati hayo yanatokea Lema alisisitiza kuwa kamwe hawezi kukubali
kutohamasisha wananchi kwenda kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la
Wapigakura licha ya kudai kuwa, kundi la vijana wanaosadikiwa kuwa wa
CCM wamempiga mawe sambamba na watu wengine waliojitokeza kujiandikisha
katika kata mbalimbali.
Hata hivyo, upande wa vijana wa CCM, umedai wenzao wa Chadema ndio
chanzo cha vurugu, kwani wameonekana wakisambaza makundi ya vijana
wasiostahili kuandikisha katika vituo mbalimbali.
Lema ajitetea
Akizungumzia kukamatwa kwake na polisi wa kata ya
Osunyai kutokana na vurugu zilioibuka, alidai alikuwa akitoa taarifa za
uongezwaji wa mashine za BVR kwa wananchi na kuwapa moyo kuwa watulivu
wakati wa uandikishwaji sambamba na kutunza vitambulisho hivyo kwa ajili
ya kupiga kura mwaka huu katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na
madiwani.
Alisema wakati akiendelea kuwapa moyo wananchi na kusema Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeongeza mashine za BVR, ghafla aliona vijana
anaodai wamekodishwa kufanya vurugu kwenye vituo mbalimbali vya
kujindikisha na ndipo alitoa taarifa Polisi, lakini badala ya kukamata
vijana hao alikamatwa yeye na vijana wengine na kuwekwa mahabusu.
NEC iliruhusu uandikishaji kuendelea hadi saa mbili usiku kutokana na
wingi wa watu wanaostahili kuandikishwa.
Hata hivyo mmoja wa wafuasi wa
CCM aliyejitambulisha kwa jina la Abdi Marijani maarufu kwa jina la
‘`Mutu’ alisema Chadema wamekuwa wakileta watu ambao sio wakazi wa Jiji la
Arusha kutaka kujiandikisha hali iliyopingwa na vijana hao.
Mutu alisema CCM ilikuwa imepewa taarifa juu ya njama za Chadema za
uchomekeaji watu katika kila kata na chama kikaweka vijana imara katika
kila kituo wakiwa na mabalozi ambao ndio wenye jukumu la kujua mkazi wa
eneo husika.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Lema alisema juzi
akiwa kata ya Osunyai alishangaa kuona kundi la vijana wakiwa kwenye
gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T 122 ATR ambalo
alidai wakati mwingine gari hilo lilibadilishwa namba na kusomeka T 122
ABR wakishuka ghafla na kuanza kumpiga mawe na kuwapiga vijana wengine
25 ambao walikuwa katika kituo hicho.
Alisema wakati tukio hilo likitokea alitoa taarifa kwa Mkuu wa
Upelelezi wa wilaya OC/CID, Faustine Mwafele ili kuwaelezea tukio hilo,
lakini polisi walifika eneo la tukio badala ya kuwakamata vijana hao
walimkamata yeye na vijana waliokuwepo kisha kuwaweka chini ya ulinzi.
Alisema inaonekana kundi hilo linaonekana lipo juu ya sheria watu
wanafanya fujo za waziwazi, huku mbunge akigeuziwa `na kusulubiwa.
Alisema kwa kuwa yeye ni mbunge, hawezi kuacha kuhamasisha wananchi
wake kujiandikisha badala yake chama chao na viongozi wa chama
wataendelea kuhamasisha watu kujitokeza kujiandikisha sambamba na
kuhamasisha watu wasikate tamaa katika kujiandikisha kwa sababu ni
wajibu wao wa kisheria, kisiasa na kidemokrasia.
Aliongeza kuwa udhalilishwaji sasa umefika mwisho, hivyo alitoa rai
kwa vijana wa chama hicho kuchukua hatua ya kuwalinda viongozi wao,
kulinda demokrasia na mali zao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas hakupatikana
kuzungumzia tukio hilo, licha ya kutafutwa kupitia simu yake ya mkono
ikiwa ni pamoja na kutumiwa ujumbe mfupi wa maandishi.
Wasemavyo CCM
Akizungumzia hilo, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Arusha,
Feruz Banno alisema vurugu zilianzishwa na vijana wa Chadema kwa
kuwapiga vijana wa CCM na kupiga risasi hewani hovyo bila ya sababu za
msingi.
Banno alisema dola Arusha inapaswa kuwa makini, kwani hali inaweza
kuwa mbaya zaidi iwapo hilo halitadhibitiwa na kuwafanya watu wengine
kushindwa kwenda kujiandikisha kwa kuogopa vurugu.
Alisema kutokana na vurugu zinazofanywa kwenye baadhi ya vituo vya
kujiandisha na baadhi ya viongozi wa Chadema ili kudhibiti wazee na
akinamama wanaokwenda kujiandikisha kwenye vituo hivyo.
Alisema kwa sasa uandikishaji unafanyika katika kata za Terati,
Murieti, Olusunyai, Moshono, Sinoni na Sokoni One, lakini baadhi ya
vijana wa chama hicho wamekuwa wakisafirishwa kwa magari kutoka kata
tofauti na hizo na kupelekwa eneo hilo kwa ajili ya kujiandikisha .
Ulinzi
Kwa upande wake Marijani, alisema kutokana na udhibiti
uliowekwa na makamanda wa CCM vituo vya kupigia kura wamebaini kuwa
viongozi wa Chadema na vijana wao wamekuwa wakileta vurugu katika kila
kituo ili zoezi hilo lisiweze kufanikiwa.
“Tumeweka ulinzi kila kituo na hiyo itakuwa ikifanyika katika kata
zote za Jiji la Arusha kwani hiyo itasaidia kupata wakazi halisi wa eneo
husika na sio mamluki,” alisema Mutu.
0 comments:
Post a Comment