BALOZI
wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Filiberto Sebregondi, ameshauri Uchaguzi
Mkuu wa mwaka huu ufanyike kwa uwazi zaidi ili kulinda amani iliyopo
nchini.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Balozi Sebregondi,
alisema pia ni lazima Serikali ifanye maandalizi ya kutosha na wagombea
washiriki kwa amani katika kipindi chote cha kampeni.
“Mwaka
huu ni wa muhimu kwa Tanzania kwa sababu inatarajia kupata viongozi
wapya kuanzia ngazi ya rais, tunaamini ni nchi inayoheshimu Katiba kwani
kiongozi akimaliza muda wake anawapisha wengine kwa mujibu wa Katiba
jambo ambalo nchi nyingine zimeshindwa kufuata utaratibu huu na kuingia
katika machafuko,” alisema.
Alisema
EU imekuwa ikishirikiana kwa ukaribu na Tanzania katika masuala
mbalimbali yakiwamo hayo ya uchaguzi ambapo mwaka 2010 ilisambaza
waangalizi wake zaidi ya 100 ambao walisimamia ili kuangalia unafanyika
kwa vigezo vya kimataifa.
“Baada
ya uchaguzi ule tulitoa mapendekezo ambayo yalitajwa pia katika Katiba
Inayopendekezwa ambayo mchakato wake umesitishwa, lakini nia yetu ni
kuona uchaguzi unaendelea kuwa huru na haki,” alisema.
Sebregondi
alitaja mapendekezo hayo kuwa ni kuwapo Tume Huru ya Uchaguzi, uhuru wa
vyombo vya habari katika kupata na kusambaza taarifa za uchaguzi kwa
umma na wananchi wapewe fursa ya kukata rufaa kupinga matokeo
mahakamani.
“Hatutamani
yale yaliyotokea Zanzibar mwaka 2010 yajirudie tena, na ndiyo maana
bado tunaendelea kusaidia ikiwa ni pamoja na kuwezesha mafunzo kwa
askari polisi juu ya namna ya kusimamia watu vizuri kwenye kipindi cha
uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani,” alisema.
Naye
Naibu Mwidhinishaji Mkuu wa Mfuko wa Fedha (EU) wa Wizara ya Fedha,
Godlove Steven, alisema tangu mwaka 2008 hadi 2013 umoja huo umeipatia
Serikali euro milioni 6.6 sawa na zaidi ya Sh trilioni moja ambazo
zimetumika katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo nchini.
0 comments:
Post a Comment