WANANCHI
wa Kijiji cha Ibondo Kata ya Katoro Wilaya ya Geita, wameifunga
zahanati ya kijijini hapo kwa madai kuwa inatoa huduma mbovu licha ya
kutoza wagonjwa fedha.
Tukio
hilo lilitokea jana ambapo baadhi ya wananchi waliozungumza na Mpekuzi
walieleza kuwa wanataka mganga mkuu na muuguzi wa zahanati hiyo
waondolewe kwa sababu wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya kazi.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo, uamuzi wa kuifunga zahanati hiyo umefikiwa kwa
sababu badala ya kutoa huduma inasababisha adha kwa wagonjwa.
Walisema
walikwishafikisha malalamiko yao kwa mganga mkuu wa zahanati hiyo
kuhusu utendaji mbovu wa muuguzi, lakini amekuwa akimkingia kifua.
“Kweli
sisi kama wananchi wa Kijiji cha Ibondo tumechoshwa na mganga na
muuguzi wa zahanati hii, wagonjwa wamekuwa wakinyanyaswa sana, tunatozwa
fedha, unapokuwa hauna fedha unaambiwa ulete kuku, bata au mbuzi, mimi
ni miongoni mwa watu tulioombwa rushwa ya kuku na wanapikiwa hapa hapa
kituoni na manyoa ya kuku yapo,” alisema Juakali Daudi.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Mzee Kelomba mwenye umri wa miaka 70 alisema: “Rushwa…
rushwa imefanya wananchi wa Ibondo tupate shida, huna pesa hakuna
huduma. Lakini kama una chochote matibabu utapata, tena haraka.
“Nilimleta
mjukuu wangu hapa apatiwe matibabu, lakini nilitazamwa kama sanamu
mpaka nikampeleka kwa waganga wa kienyeji, matibabu kwa wazee ni tete
tunahangaishwa sana.”
Muda mfupi baadaye, askari wa kituo kidogo cha polisi cha Katoro walifika na kuvunja kufuli lililokuwa limewekwa na wananchi.
Pia walimkamata Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Lubadisha Sindano anayedaiwa kuhamasisha wananchi kuvamia zahanati na kuifunga.
Akijibu
tuhuma za kupokea rushwa na kutoa huduma mbovu, muuguzi Justina Joseph,
alisema kuwa tuhuma hizo si za kweli na kwamba mgogoro uliopo ni chuki
za watu binafisi zinazosababishwa na masuala ya kisiasa.
Naye
Mganga wa Zahanati hiyo, Asteria Nshekinabo, alikiri kufungwa kwa kituo
hicho huku akitolea ufafanuzi suala la kutozwa fedha wagonjwa ambapo
alisema wanaotozwa pesa ni wale ambao hawajajiunga na Mfuko wa Bima ya
Afya (CHF).
0 comments:
Post a Comment