KATIBU
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, leo anatarajia
kuanza ziara ya siku kumi mkoani hapa, kukagua utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi na kuimarisha uhai wa chama.
Taarifa
iliyotolewa na Katibu wa CCM Mkoa Mwanza, Miraji Mtaturu kwa waandishi
wa habari, imeeleza kuwa Kinana ataanzia ziara yake katika Kijiji cha
Nyamadoke, Wilaya ya Sengerema akitokea mkoani Geita.
“Ziara
ya Katibu Mkuu Kinana akiwa mkoani Mwanza itakuwa ya kihistoria kwa
sababu atafika kwenye baadhi ya maeneo ya wilaya za Ukerewe na Misungwi
ambayo viongozi wa CCM kitaifa na Serikali hawajawahi kufika tangu
kupatikana kwa uhuru wa taifa hili.
“Ni
lengo sisi kama chama kuitumia ziara hiyo kurejesha hamasa kwa wana CCM
ili tuweze kuyarudisha majimbo ya ubunge yaliyochukuliwa na upinzani
mwaka 2010,” alisema Mtaturu.
Aliyataja
baadhi ya maeneo ambayo Kinana atafika na kuwa kiongozi wa kwanza wa
kitaifa wa CCM kuyatembelea kuwa ni Kisiwa cha Ilugwa kilichopo wilayani
Ukerewe ambapo atashiriki ujenzi wa kituo cha afya na baadaye ataelekea
Kijiji cha Mahando, wilayani Misungwi atakakoweka jiwe la msingi la
ujenzi wa ofisi ya CCM kabla ya kupokea wanachama wapya na kuwakabidhi
kadi.
Mtaturu alizitaja wilaya ambazo Kinana atazitembelea kuwa ni Kwimba, Magu, Nyamagana, Ilemela na Ukerewe.
0 comments:
Post a Comment