Pages

Ads 468x60px

Thursday, July 9, 2015

Dewji Atangaza Kutogombea Tena Ubunge Singida Mjini >>


Mbunge wa Singida Mjini (CCM) na mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji amewaliza baadhi ya wapigakura wake wakati akitangaza kutogombea tena nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa ya madai ya kubanwa na majukumu ya kifamilia na biashara. 
 
Dewji ambaye amekuwa mwakilishi wa jimbo hilo kwa awamu tatu mfululizo, alitangaza uamuzi wake huo kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi.
 
Alisema kuwa aliomba ridhaa ya kuwatumikia wananchi wa Singida Mjini mwaka 2000, hakuwa na familia na pia biashara zake hazikuwa kubwa kama ilivyo sasa.
 
Alisema katika kipindi chote cha uwakilishi wake, wakazi wa Singida Mjini wamempa heshima kubwa, ukarimu wa hali ya juu, wema uliotukuka na uvumilivu usio na kifani na kwa hali hiyo, hatawasahau kamwe na ataendelea kuwatumikia kupitia mfuko maalumu aliouanzisha.
 
Aliwataka wakazi hao kuendeleza moto wa maendeleo waliouwasha miaka 10 iliyopita kwa miaka mingine kama hiyo ijayo ili jimbo hilo lipige hatua zaidi.
 
“Kwa kutambua heshima mliyonipa na imani kubwa mliyonionyesha kwa vipindi vyote vya uongozi wangu, ingawa nina huzuni lakini sina budi niwaombe kuwa mwaka huu wa uchaguzi sigombei tena na ninatoa fursa kwa kada mwingine wa CCM anipokee kijiti hiki kuliongoza jimbo letu,” alisema kwa huzuni. 
 
Baada ya kutamka maneno hayo, wananchi wengi katika walipiga kelele kwa nguvu wakionyesha kutokubaliana na uamuzi wake. Huku moja ya sauti ikisikika... “Hatutaki mbunge mwingine ni wewe tu hadi tukuchoke.”
 
Awali, Dewji alitaja baadhi ya maendeleo yaliyofanyika katika vipindi vyake, kuwa ni pamoja na kujenga shule 15 za sekondari kutoka mbili zilizokuwapo.
 
Alisema kwa kutumia fedha zake alijenga na kuchimba visima 45 vya majisafi na salama.

0 comments:

Post a Comment

SHARE