Wakati Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari akisema anashindwa kuamini kilichotokea na kunusurika katika ajali ya helikopta juzi, mmiliki wa chopa hiyo, Philemon Ndesamburo amesema atanunua nyingine haraka kabla ya kuanza kampeni za Uchaguzi Mkuu.
Kauli hizo zilitolewa jana ikiwa ni siku moja
baada ya helikopta hiyo inayomilikiwa na Ndesamburo kupitia kampuni yake
ya Keys Aviation kupata ajali wakati ikitumiwa na Nassari na baadhi ya
viongozi wa Chadema.
Wakati ikipata ajali, ilikuwa imekodishwa na Kampuni ya General Aviation Services (T) Ltd inayomilikiwa na Kapteni William Slaa.
Katibu wa Ndesamburo, Basil Lema alisema ilipata
ajali baada ya kupigwa na kimbunga wakati anga likiwa limefunikiwa na
wingu zito.
“Mheshimiwa Ndesamburo amemshukuru Mungu kwa
kuwanusuru watu waliokuwa kwenye ndege hiyo ambao ni pamoja na Mbunge
Joshua Nassari.
“Ameweka wazi kwamba atalazimika kununua nyingine
mapema kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka
huu,” alisema Lema akimnukuu Ndesamburo.
Lema alisema rubani aliyekuwa akiendesha helikopta
hiyo alifanikiwa kuielekeza juu ya miti alioutumia kupunguza kasi ya
kushuka chini na kusaidia abiria kutoka salama.
“Imeharibika lakini abiria wote ni wazima.
Walikuwamo wanne,” alisema na kuongeza kuwa helikopta hiyo ndiyo
iliyotumiwa na Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 na Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa mwaka jana na chama hicho kilitegemea kuitumia katika
Uchaguzi Mkuu ujao.
Pia, imewahi kutumiwa na makada mbalimbali wa CCM
akiwamo Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba na kada maarufu wa
Moshi mjini, Buni Ramole.
Kauli ya Nassari
Akizungumza na waandishi wa habari katika wodi
alikolazwa kwenye Hospitali ya Seliani – Arusha, Nassari alisema
waliporuka kutoka Leguruki, hakukuwa na dalili zozote za kuchafuka kwa
hali ya hewa, lakini dakika chache baada ya kuruka angani wingu zito
lililoambatana na upepo mkali liliwafunika ghafla.
“Wingu lile na upepo ule sijawahi kuona katika
maisha yangu yote zaidi ya kusoma kwenye vitabu vya simulizi vya mambo
ya ushirikina. Namshukuru Mungu wote tuko salama kwani hatukuwa na
matumaini ya kupona ajali ile,” alisema Nassari.
Mbunge huyo aliyekuwa katika ziara ya kuhamasisha wananchi
kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura, alimwagia sifa rubani Slaa
kwa uwezo na ustadi aliouonyesha hadi wakanusurika.
“Kama siyo ustadi wake, naamini watu wangeokota
vipande vya nyama tu kwenye eneo la ajali, ila Mungu ni mkuu leo tuko
hai wote licha ya madhara madogo,” alisema.
Nassari alisema muda mfupi kabla ya kuruka saa
kumi na moja jioni, wakati akihutubia mkutano huko Leguruki, alipokea
simu kutoka kwa mchungaji mmoja akimtaarifu kupata maono kuwa
anakabiliwa na hatari ya kukutwa na jambo kubwa na baya akimtaka adumu
katika sala.
“Dakika 15 baadaye nikaruka na kupata ajali.
Naamini kilichotuokoa ni nguvu ya sala niliyosali baada ya kupokea
ujumbe wa mchungaji na maombi ya wachungaji wangu wanaoniombea kila
siku,” alidai Nassari.
Rubani Slaa alisema alishangaa lilipotokea wingu
na upepo uliosababisha ndege kuanguka ikiwa njiani kuelekea Ndoombo na
Ngureserosambu.
“Kabla ya kurusha ndege nilijiridhisha na hali ya
hewa. Hakukuwa na kiashiria chochote cha hali ya hatari kama maeneo
mengine ambako tulishindwa kutua kutokana na mvua zilizokuwa zikinyesha."
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Seliani, Dk Paul
Kisanga alisema hali za majeruhi si mbaya, isipokuwa Eva Kayaha
aliyevunjika mbavu mbili.
0 comments:
Post a Comment