Waziri mkuu Mizengo Pinda amekataa ombi la wananchi wa jimbo lake la uchaguzi la Katavi la kumtaka agombee tena ubunge katika jimbo hilo ili kuendeleza mipango mbalimbali ya maendeleo aliyoianzisha.
Akizungumza
baada ya Ibada ya Jumapili katika kigango cha Kanisa Katoliki cha
Kibaoni wilayani Mlele (Jumapili, Julai 19, 2015), Waziri Mkuu Pinda
amesema anamshukuru Mungu kwa nafasi aliyopewa ya kulitumikia Taifa
akiwa Waziri Mkuu kwa miaka minane na anaamini wakati umefika wa yeye
kuwaachia wengine nafasi ya ubunge wa jimbo la Katavi.
Amesema
yeye ataendelea kuwa karibu na wananchi wa Katavi wakati wote na kwa
vile atakuwa na muda wa kutosha atashiriki kikamilifu katika mikakati
mbalimbali ya kuwaletea maendeleo wananchi ili waweze kujikwamua kutoka
kwenye umaskini.
Mheshimiwa
Pinda aliwaasa wananchi wa jimbo la Katavi wawe makini katika kuchagua
mbunge na madiwani na kamwe watoa rushwa na wabadhirifu wasipewe nafasi
katika uchaguzi ujao.
Akimshukuru
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Paroko wa Parokia ya Usevya wilayani Mlele,
Padri Aloyce Nchimbi aliwaasa wananchi wa Wilaya ya Mlele kumuenzi
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda hata atakapokuwa amestaafu kwani
bado watahitaji busara na uzoefu wake katika kujiletea maendeleo.
Waziri Mkuu yuko kijijini kwake Kibaoni, wilayani Mlele kwa ajili ya mapumziko mafupi.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 19, 2015.
0 comments:
Post a Comment