WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya, anatarajia kuchukua fomu kuwania urais Juni tatu mwaka huu.
Mwandosya ambaye tayari ametangaza kuacha kuwani ubunge katika Jimbo
la Rungwe Mashariki, anakusudia kutangaza nia yake ya kusaka safari ya
kuelekea Ikulu, Juni Mosi, mwaka huu.
Akizungumza na Mtandao huu jana nje ya viwanja vya Bunge, Profesa
Mwandosya alisema sababu zilizomsukuma kuwania urais, atazitaja Juni
Mosi atakapotangaza nia mkoani Mbeya.
” Sababu za kutaka kuwania urais na nini nitawafanyia Watanzania,
nikiingia madarakani nitaeleza siku ya kutangaza nia Juni Mosi,” alisema
Profesa Mwandosya.
Waziri Mwandosya ni mmoja kati ya makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM)
ambao kwa muda mrefu wameonesha nia ya kutaka kumrithi Rais Jakaya
Kikwete anayemaliza muda wake.
Ikumbukwe kuwa Waziri Mwandosya alipata kuwania urais mwaka 2005 na
aliingia kwenye kundi la tatu bora miongoni mwa wagombea 11 waliowania
nafasi hiyo.
Walioingia tatu bora mbali ya Profesa Mwandosya ni pamoja na Dk.
Salim Ahamed Salim na Rais Jakaya Kikwete ambaye aliibuka mshindi.
Mwandosya amewahi kuwa waziri katika wizara mbalimbali katika Serikali za awamu tofauti tofauti.
Hatua hiyo ya kutangaza nia imekuja baada ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), kutangaza ratiba ya wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya chama
hicho kuanza kuchukua na kurejesha fomu.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, wagombea wa nafasi ya urais muda wa
kuchukua fomu ni Juni 3 hadi Julai 2, muda ambao utatumiwa sambamba na
kazi ya kutafuta wadhamini mikoani.
0 comments:
Post a Comment