Nyota ya Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa, imeendelea kung’aa baada ya Taasisi ya Samunge Social Sciences Research Center (SSSRC), kufanya utafiti na kubaini kuwa kiongozi huyo ni chaguo la kwanza kwa wananchi.
Utafiti
huo uliofanywa miaka miwili kuanzia 2013 hadi 2015, unaonyesha Lowassa
anaongoza kwa asilimia 20.7 dhidi ya wagombea 31.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mtafiti Mkuu wa
SSSRC, George Nyaronga, alisema utafiti huo waliufanya kwa kutumia
madodoso pamoja na mahojiano kwenye mikoa 18.
Utafiti
huo na asilimia walizopata wanasiasa wengine kwenye mabano ni Katibu
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema, Dk. Willbrod Slaa
asilimia 11.7; Waziri wa Ujenzi, John Magufuli (7.6); Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (7); Naibu Waziri wa
Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba (4.8);
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba (4.2)
na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe 3.4 sawa na Kiongozi Mkuu wa ACT
Wazalendo, Zitto Kabwe.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (2.4) na Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia (1.2).
Alisema pia utafiti huo ulionyesha kuwa Lowassa pekee ndiye anayekubalika na wapiga kura wengi, karibia idadi sawa ya jinsia zote mbili, wanaume 50 na wanawake 49.
Kwa
ujumla, Lowassa na vinara wengine 10 wanaotajwa kuwania urais walipata
asilimia 67.2, huku asilimia zilizobaki (32.8) zikitwaliwa na wagombea
wengine 10 kati ya 20 waliohusishwa katika utafiti huo.
Aidha,
Nyaronga alisema hawakuwa na dodoso linaloorodhesha majina ya
wanaopendekezwa kuwa Rais ila majina yalitajwa na wajaza madodoso
wenyewe kisha wao wakajaza majina kwenye SSSRC.
Kwa
mujibu wa dodoso lenye kichwa cha habari cha katika tafiti kuhusu
uchaguzi wa mwaka 2015, takwimu zinaonyesha kuwa Watanzania wanamtaka
mtu mwenye kufanya maamuzi magumu.
Alisema
kwa maoni ya wengi waliohojiwa na kujaza dodoso, wanaonyesha kuwa
Lowassa anakubalika zaidi na kwamba ulifanywa katika mikoa 18 ya Bara na
Visiwani, watu 1,000 walijaza dodoso na 6,000 walifanyawa mahojiano.
Alisema
utafiti huo uliofanywa kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Zanzibar,
Morogoro, Singida, Shinyanga, Mwanza, Mara, Mbeya, Katavi, Kigoma,
Tabora, Arusha, Moshi, Iringa, Njombe, Songea, Lindi na Mtwara .
Nyaronga
alisema baadhi ya mambo ambayo tafiti hiyo ilikuwa ikitafuta majibu ni
masuala yanayohusu changamoto kwa Tanzania kwa sasa, sifa za kiongozi
anayehitajika kukabiliana na changamoto hizo, mapendekezo ya jina la
Rais atakayesimamia vizuri changamoto hizo, chama chenye uwezo wa
kutupatia rais ajaye kwa mujibu wa katiba ya mwaka 1977 na kama
Watanzania watapiga kura.
Vyama vya Siasa
Alisema utafiti huo umebaini CCM ina asilimia 53.5 ya kutoa Rais , Chadema yenye asilimia 34.2.
Alisema
vijana wa miaka kati ya 18-25 ambao ni sawa na asilimia 46 wanamtaka
Lowassa kuwa Rais, ikifuatiwa na vijana wa miaka 26-30, na vijana wa
kati ya miaka 30-35.
Aliongeza
kuwa CCM kina wanachama wengi wenye umri mdogo ikilinganishwa na vyama
vingine vya siasa Tanzania na Chadema ndicho kinachofuatia kwa kupendwa
na umri wa miaka kati ya 18 -25.
Mtafiti
huyo alisema CCM inapendwa zaidi na watu wenye aina mbalimbali za elimu
kuanzia shahada ina watu 144, sekondari ina watu 84 na hata katika
elimu ya msingi ina watu 18, ikifuatiwa na Chadema.
Alizitaja
changamoto kuu 16 zilizopo Tanzania kwa sasa kama zilivyoorodheshwa na
wananchi ambapo wanamtaka Rais ajaye azishugulikie ni elimu, afya,
viwanda, ajira, kilimo, miundombinu hafifu, kukosekana kwa utawala bora,
uchumi hafifu, nishati, migogoro ya ardhi, mikataba mibovu.
Nyingine ni ukwepaji kodi, rushwa, ufisadi, ubinafsi na kutokuwa na uzalendo.
“Katika
tafiti hii tumegundua kuwa Lowassa anaongoza katika kila nyanja kama
Rais pendekezwa kuwa Rais wa Tanzania 2015, ukiangalia jinsia zote wa
kiume na wa kike wanamtaka Lowassa kuwa Rais,” alifafanua na kuongeza:
“Tafiti
hii inaipa chama dira na mwelekeo wa kujua kwamba ni Mtanzania gani
ndani ya chama anayehitajika na Watanzania, chama kikishajua hilo
hakifanyi kosa kumwacha mtu huyo anayehitajika na Watanzania ili kwanza
kukiokoa chama kupoteza dola lakini pia kukilinda kiweze kubaki
madarakani.”
Aliasema
chama mbadala wa CCM ni Chadema, takwimu zinaonyesha kuwa, iwapo
Lowassa hatapeperusha bendera ya CCM 2015, basi anayetakwa na wananchi
kuwa Rais mbadala ni Dk. Willibrod Slaa.
Alisema
Machi 2015, taasisi isiyo ya kiserikali ya Positive Thinkers Tanzania
ripoti yake ya utafiti ilioji watu 3,298 na Lowassa alipata watu 752
katika mikoa 13 Tanzania Bara na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo,Tibatizibwa
Yabutinga, alielezea kuwa Lowassa ni mwanasiasa anayekubalika sana kuwa
rais ajaye 2015.
Alisema
katika ripoti hiyo ili orodhesha matokeo yake kuwa Lowassa alipata
asilimia 22.8, Slaa 19.5 asilimia , Nchemba 10.6, Profesa Lipumba 8.9,
John Magufuli 6.8 , Kabwe 6.7, Membe 5.9, Pinda 3.2 , makamba 1.6,
Mwandosya 1.2.
Alisema
Twaweza sauti za Wananchi, Nov.2014 Imegundua kuwa katika watu 1,445
walioshiriki utafiti ni kuwa wengi wao walisema kuwa changamoto kuu ni
Uchumi, elimu na afya na wanasiasa wengi hawatimizi ahadi zao.
Twaweza
pia wametoa tafiti kuwa CCM bado kinapendwa na Watanzania kwa asilimia
51 kwa nafasi ya urais, asilimia 46 kwa nafasi ya ubunge na kwa asilimia
47 kwa nafasi za udiwani ikifuatiwa na Chadema.
Alisema
ripoti hiyo ya Twaweza pia inatoa ripoti kuwa vijana chini ya miaka
34, watu chini ya miaka 50 na wazee zaidi ya miaka 50 kwa pamoja wengi
wana sapoti kubwa kwa chama cha mapinduzi, na katika nafasi ya urais
2015, ripoti ya Twaweza inasema kuwa ndani ya CCM, kura za wagombea
urais kwa tiketi ya CCM ni Lowassa anaongoza kwa asilimia 17, Pinda
asilimia 14, Magufuli asilimia tano, Samuel Sitta asilimia tano, Membe
asilimia saba.
Alisema
ripoti hiyo ya Twaweza pia iliweka wazi kuwa iwapo uchaguzi utafanywa ,
basi CCM itaongoza kwa asilimia 47, Ukawa kwa asilimia 28 na kama mtu
atasimama binafsi, basi atapata asilimia 19.
0 comments:
Post a Comment