Rais
Kikwete amewaongoza watanzania katika maadhimisho ya siku ya kupinga
matumizi ya dawa za kulevya duniani yaliyofanyika kitaifa mjini Bagamoyo
katika viwanja vya shule ya msingi Mwanamakuka.
Shughuli
hizo zilianza kwa maandamano katika viwanja hivyo ambapo badaye mkuu wa
mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alimkaribisha Rais pamoja na
wananchi waliohudhuria katika viwanja hivyo.
Katika
hotuba yake, Rais Jakaya kikwete alisema vita dhidi ya madawa ya
kulevya ni kubwa na inahusisha wafanyabiashara wakubwa ambapo fedha
zinazopatikana hutumika kufadhili uhalifu wa kimataifa ikiwemo ugaidi.
Rais
Kikwete alisema anajivunia kutungwa kwa sheria mpya ya kudhibiti na
kupambana na dawa za kulevya ya mwaka 2015 katika serikali ya awamu ya
nne, ambayo inaweka masharti ya kuundwa kwa chombo maalum
kitakachoshughulikia kwa ukaribu tatizo hilo, na kwamba anataka chombo
hicho kiwe kimeundwa kabla ya Oktoba ili kutoa baraka zake kabla
hajaondoka madarakani, na atamkabidhi Rais ajaye aendelee kuanzia hapo.
Awali
Waziri wa Afya na ustawi wa jamii, Dkt Seif Rashid alipata fursa ya
kufafanua mikakati ya serikali katika kupambana na tatizo la matumizi ya
madawa ya kulevya na kuwapiga vita wafanyabiashara wanaojihusisha na
dawa hizo.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi isiyokuwa ya serikali inayojishughulisha
na masuala ya vijana Tanzania Youth Aliance TAYOA, Peter Masika alisema
kwamba wamezindua namba ya simu itakayotumika kuwaelimisha vijana dhidi
ya athari ya matumizi ya madawa ya kulevya.
Wakati
huo huo mwanaharakati anayepambana na matumizi ya madawa ya kulevya
Rehema Chalamila – Ray C aliwataka vijana wenzake waliojitumbukiza
katika janga hili waweze kufuata mfano wake na wajitokeze kutokomeza
janga hili kwa kutumia dawa za Methadoni na kuacha kabisa madawa.
Katika
maadhimisho hayo ambayo yaliyoongozwa na kauli mbiu ya tujenge jamii na
maisha ya utu bila dawa za kulevya, Rais kikwete alihimiza ushirikiano
kwa jamii katika kupinga matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana na
kutokomeza biashara hiyo ikiwemo utoaji wa elimu ya kutosha kwa jamii
ili kuwasaidia vijana walioathirika na dawa za kulevya.
0 comments:
Post a Comment