WANAFUNZI
sita wa Sekondari ya CTC Kigonsera inayomilikiwa na Misheni ya Mbinga
mkoani Ruvuma na Mkuu wa Shule hiyo, Padre Yazint Kawonga, wamefariki
dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutumbukia bondeni kisha
kuwaka moto na kuiteketeza miili yao.
Akizungumza
na Mpekuzi jana shuhuda wa ajali hiyo, Makarius Nchimbi, alisema
ilitokea juzi saa tisa alasiri katika mlima uliopo karibu na shule hiyo
huku likiwa limewabeba wanafunzi waliokuwa wakitokea shambani kuvuna
mahindi ya shule hiyo.
Nchimbi
ambaye ni mfanyakazi wa kitengo cha udereva katika misheni hiyo alidai
yeye ndiye aliyekuwa dereva wa gari hilo kabla ya kupokelewa na Padre
Kawonga aliyemtaka amsaidie kuliendesha kwa kuwarudisha shuleni
wanafunzi waliokuwa shamba lililopo Kijiji cha Mkulumus kilichopo
Kigonsera.
Alisema
gari hilo aina ya Land Rover 110 Station Wagon lenye namba T 306 AYM
lilipofika katika mlima huo lilimshinda Padre Kawonga wakati akitumia
gia namba mbili na kuanza kurudi nyuma huku wanafunzi wengine waliokaa
juu walifanikiwa kuruka kabla halijatumbukia na baadhi yao 24 waliumia.
Alisema
baada ya gari hilo kutumbukia bondeni wao walijitahidi kuingia kwenda
kuvunja milango ili waweze kuwaokoa baadhi yao lakini ilishindikana
kutokana na nyaya za umeme wa gari kulipuka na kuliunguza huku miili yao
ikiwemo ndani na kusababisha ishindwe kutambulika.
Alisema
kutokana na moto kuwaka iliwalazimu watafute mbinu za kuuzima na
walitumia maji lakini haikuwezekana na walifanya jitihada ya kuipata
winchi iliyoweza kwenda kuliinua gari hilo likiwa limeteketea.
Kwa
upande wake, Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya cha Kigonsera, Dk. Patrik
Mhagama, alisema kituo hicho kilipokea maiti saba na majeruhi wakiwa 24
na kati ya hao wawili wamepekwa Hospitali ya Mbinga kutokana na hali zao
kuwa mbaya huku 17 walitibiwa na kuruhusiwa na watano bado wapo kituoni
hapo.
Naye
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikihela, alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na alisema taratibu za kuyapata majina halisi ya
marehemu bado zinaendelea na zikikamilika zitatolewa taarifa.
Aliwataja
majeruhi hao kuwa ni Japheth Komba (16), Regobert Mahai (16), Edgar
Maseko (16), Luiza Mbunda, Afa Kifaru (15), Nelalfred Nchimbi (16),
Teodora Wolfa (16).
0 comments:
Post a Comment