RAIS
Jakaya Kikwete amekiri kuwapo mazingira mabovu ya Jeshi la Magereza
nchini na kulitaka jeshi hilo kubuni njia za uzalishaji wa bidhaa zao
zitakazoweza kuwaletea faida na taifa kwa ujumla.
Aliyasema
hayo jijini Dar es Salaam jana kwenye sherehe za kumaliza kozi kwa
maofisa 104 wa ngazi ya juu wa Jeshi la Magereza yaliyofanyika katika
Chuo cha Taaluma na Urekebishaji Ukonga.
Alisema
mazingira mabovu yanachangiwa na wingi, msongamano wa wafungwa na
watuhumiwa katika magereza hali inayofanya jamii kuwa na malalamiko ya
mara kwa mara.
“Kila
mwaka wanaotetea haki za binadamu wanapopita kwenye magereza zetu,
tunakuwa tunashindwa kwenye suala la msongamano ndani ya gereza na hii
inaonyesha magereza tulizonazo 126 hazitoshelezi kulingana na kasi ya
ongezeko la uhalifu.
“Hii
inajidhihirisha wazi kwani kila inapofika sikukuu za Muungano Aprili
26, tunasamehe wafungwa, lakini ikifika Desemba 9 Sikukuu ya Uhuru
unakuta wameongezeka mara mbili,” alisema Rais Kikwete.
Alisema
ili jeshi liweze kutimiza majukumu yake vizuri, ni lazima kuwe na watu,
ujuzi na vitendea kazi ambavyo bado vimeonekana kuwa ni changamoto kwa
jeshi hilo.
Pamoja na hali hiyo alilitaka Jeshi la Magereza kuwa na malengo ya kuboresha viwango bora.
“Jeshi
linasifika kwa kuzalisha chakula na bidhaa bora, lakini kwenye
uzalishaji wenu msiishie kweye mazao ya chakula, bali muangalie na mazao
ya thamani pamoja na kuanzisha viwanda vikubwa na kilimo cha
umwagiliaji,” alisema Rais Kikwete.
Aidha
alilitaka jeshi hilo kuhakikisha linaharakisha mchakato wa Sera ya
Taifa ya Magereza na mpango kazi wake ambao ameutaka uwasilishwe kabla
hajaondoka madarakani Oktoba mwaka huu.
Awali
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Minja, alisema jeshi hilo
linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo la ongezeko la mahabusu,
upungufu wa fedha kutokana na gharama kubwa ya uendeshaji, makazi ya
maofisa na askari, ofisi chakavu na suala la usafirishaji.
“Mazingira
yetu hayaridhishi sana, nyumba ni chache na zilizopo ni chakavu, pia
magari kwa ajili ya usafirishaji bado ni tatizo sambamba na majengo
machache ya mahakama,” alisema Kamishna Minja.
0 comments:
Post a Comment