Ofisa mmoja wa CCM makao makuu mjini hapa, alisema kuwa
wanachofanya wao kama watendaji ni kuandaa majina ya wagombea wote na
fomu zao za udhamini na kisha kukabidhi kwa sekretarieti itakayopanga
ajenda za vikao vya Kamati Kuu na baadaye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)
ya taifa.
Ofisa huyo alipoulizwa kama ana taarifa za kuwako kwa
mizengwe dhidi ya Lowassa alisema kwa ujumla kwa sasa kuna maneno mengi
sana yanazungumzwa juu ya mchakato wa uteuzi wa mgombea, ila akasisitiza
kuwa la msingi ni kusubiri vikao vya maamuzi.
“Ndugu yangu ukiyatazama haya makundi (ya urais) ni vigumu kuamini kama wanatoka chama kimoja. Yaani kuna kukamiana kweli kweli…Kila mmoja anataka kumwangusha mwenzake ili yeye apite,” alisema na kuongeza kuwa:
“Hata kama kuna mizengwe, si unajua uchaguzi huu ni wa
vyama vingi. CCM haishindani pekee yake, kwa hiyo mgombea anayekubalika
ndiye anatakiwa.”
Hata hivyo, kwa muda sasa kumekuwa na mfululizo wa habari
za kupikwa kwamba jina la Lowassa litaishia Kamati Kuu kwa madai kwamba
kuna ushahidi wa matumizi ya fedha kwa timu yake, tuhuma ambazo binafsi
(Lowassa) amezikanusha mara kadhaa.
Julai mosi mwaka huu siku anarejesha fomu za kuwania urais
kupitia CCM alitoa changamoto kwa yeyote mwenye ushahidi wa kuhusika
kwake na rushwa ajitokeza na kusema alitoa lini, wapi na kwa nani.
Lowassa alisema amechoka kwa tuhuma za kipuuzi za
kuhusishwa na rushwa na kusisitiza kuwa hakuna mwanachama yeyote
miongoni mwa zaidi ya nane waliomdhamini aliyefanya hivyo kwa kishawishi
cha fedha au fadhila yoyote.
Mgombea anayetajwa kutumiwa zaidi na kundi linalompinga Lowassa ni pamoja na Makongoro Nyerere, ambaye alifanya mkutano na waandishi wa habari hivi karibuni na kuporomosha kauli kali za ukakasi dhidi ya Lowassa.
Wakati mizengwe ikizidi kusukwa dhidi ya Lowassa, ripoti ya
kura zote za maoni ambazo zimekuwa zikitolewa katika miezi ya hivi
karibuni zimeonyesha kuwa Lowassa anaongoza kwa mbali kama chaguo la
wananchi wengi kwenye nafasi hiyo.
Miongoni mwa tafiti hizo ni ule wa Mpango wa Utafiti na
Elimu ya Demokrasia (REDET) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, uliofanywa
mwezi uliopita na matokeo yake kutolewa mwishoni mwa wiki unaonyesha
kuwa Lowassa ni changuo la kwanza la wengi kwa kujipatia asilimia 27.0
ndani ya chama hicho, huku Bernard Membe akishikilia nafasi ya pili kwa
kupata asilimia 8.2.
Katika utafiti huo ambao REDET walisema kuwa unaweza
kuchukuliwa kwa ujumla wake kama maoni ya Watanzania endapo masuala
yaliyoulizwa uchaguzi ungefanyika katika kipindi cha utafiti, wahojiwa
walikuwa 1,250 kutoka wilaya moja moja katika mikoa 25 ya Tanzania Bara.
Wakati mkakati wa mizengwe ukiendelea kupamba moto, wajumbe
wa sekretarieti ya Kamati Kuu ya chama hicho wanaanza vikao mjini
Dodoma leo kundaa pamoja na mambo mengine ajenda na taarifa kwenye vikao
vya Kamati Kuu itakayokaa Alhamisi mjini hapa.
Kikao cha Kamati Kuu kinatarajiwa kuchuka majina ya watia
nia 38 waliojitokeza kutafuta ridhaa ya chama hicho na kubakisha majina
matano tu yatakayopelekwa NEC kwa kupigiwa kura.
NEC inayotarajiwa kukutana Ijumaa wiki hii, itatoa majina
matatu kwenda Mkutano Mkuu unaotarajiwa kukutana Jumamosi kwa ajili ya
kupata jina moja la mgombea urais wa CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba
25, mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment