WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ametangaza rasmi kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema kwa kuwa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kimetangaza rasmi kwa wanachama wake wenye sifa kujitokeza kuwania
nafasi hiyo kubwa ya uongozi nchini, ameona hana budi kutangaza rasmi
azma yake.
Dk. Magufuli, mmoja wa mawaziri ambao
kwa muda mrefu wamehusishwa kwenye kinyang’anyiro cha nafasi hiyo,
alisema anaingia kwenye mchuano huo akiwa na sifa zote stahiki za kupiga
na kupigiwa kura.
Alitangaza azma yake nje ya ukumbi wa
Bunge mjini Dodoma, muda mfupi baada ya kumalizika kipindi cha maswali
na majibu bungeni, jana asubuhi.
Baada ya kuulizwa kama ana mpango huo,
mara moja alisema: “Swali hili nimeulizwa mara nyingi. Mara zote
nimekataa kulijibu kwa sababu chama chetu (CCM) kuna utaratibu wake wa
namna ya kuomba nafasi ya uongozi. Muda ulikuwa haujawadia.
“Lakini utakumbuka wiki hii hapa hapa
Dodoma, vikao vya juu vya chama chetu vimetoa ratiba kwa wanaotaka
kuwania nafasi mbalimbali kujitokeza.
“Kwa
maana hiyo sasa niko huru kujibu swali lako kwa kusema rasmi
‘nitagombea urais’. Nafanya hivyo kwa sababu naamini ninazo sifa za
kuchagua na kuchaguliwa kama mwanachama wa CCM kwa nafasi yoyote
inayojitokeza kulingana na Katiba ya chama chetu na pia Katiba ya nchi,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema siku ya kuchukua fomu
ataitangaza baadaye pindi akishakamilisha taratibu za namna ya kuanika
hadharani mambo anayokusudia kuyatekeleza endapo wana CCM watampa ridhaa
ya kupeperusha bendera ya chama hicho.
0 comments:
Post a Comment