MFANYABIASHARA maarufu wa madini ya tanzanite jijini Arusha, Mathias Manga amepigwa risasi nyumbani kwake juzi usiku na watu wasiojulikana. Polisi imethibitisha tukio na kwamba majeruhi anaendelea vizuri na matibabu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha
Liberatus Sabas alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa Manga
amepigwa risasi ubavuni saa 4.45 usiku nyumbani kwake Ngarenaro
alipokuwa anarejea katika shughuli zake.
Sabas alisema kwa mujibu wa maelezo ya Manga aliyeongea nao kwa njia
ya simu alisema kuwa wakati anarudi nyumbani kwake Ngarenaro kulikuwa na
gari aina ya Toyota Landcruiser Vx ambayo haikuitambua namba ilikuwa
ikimfuatilia nyuma kwa muda mrefu.
Alisema mara baada ya kufunguliwa mlango wa geti wa nyumbani kwake
watuhumiwa hao waliingia kupitia geti dogo lililokuwa wazi mpaka ndani
na kuanza kumshambulia kwa risasi.
Kamanda Sabas alisema katika kujiokoa Manga alitoa bastola yake na
kuanza kupambana nao kisha majambazi hao kukimbia wakimwacha akiwa
amejeruhiwa kwenye mbavu.
Alisema Manga alikimbizwa katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa
ajili ya matibabu na aliruhusiwa usiku huo huo na kurudi nyumbani kwake
kwa kuwa hali yake haikuwa mbaya sana.
‘’Manga amepigwa risasi ya kuparazwa ya ubavuni lakini hali yake
inaendelea vema sana na yuko nyumbani kwake amepumzika”, alisema.
Sabas alisema polisi inafanya uchunguzi wa tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwasaka wale wote waliohusika ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Sabas alisema polisi inafanya uchunguzi wa tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwasaka wale wote waliohusika ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Tukio hilo limeonesha kusikitisha baadhi ya wafanyabiashara wa madini
Jijini Arusha na kusema kuwa polisi inapaswa kulifanyia kazi tukio hilo
ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kali.
0 comments:
Post a Comment