WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya
amemuomba mgombea mwenzake katika kinyang’anyiro cha kutafuta ridhaa ya
kuteuliwa kuwa mgombea kupitia CCM, Edward Lowassa asisite kumuunga
mkono kama walivyofanya watangaza nia wengine ili mambo yaishe mapema.
Aidha, amewaonya wanaotishia kukihama chama endapo hawatapitishwa,
akisema huo ni upuuzi na pia vitisho kwa Mwenyekiti wa Chama na wanaCCM
kwa ujumla, hivyo wanaojiona wao ni maarufu kuliko chama wanajidanganya.
Mwandosya alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wilayani Mbozi
alipokuwa akizungumza na wanaCCM waliomdhamini katika mbio zake za
urais, pamoja na wanachama wengine waliojitokeza katika Ofisi za CCM
Wilaya.
Mgombea huyo alisema amefarijika kusikia anaungwa mkono na wagombea
wenzake, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe pamoja na kupata taarifa za
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira naye kusema
anamuunga mkono.
Alisema pamoja na kuungwa mkono na wenzake hao watatu, anamuomba pia
Lowassa naye kumuunga mkono ili kuipunguzia kazi Halmashauri Kuu ya
Taifa (NEC) ya CCM).
“Nimesikia Membe amesema hapa Mbeya asipopitishwa yeye basi atamuunga
mkono Profesa Mwandosya, nikasikia tena na Waziri Mkuu akisema hata
kama asipopitishwa yeye atafarijika kama Profesa Mwandosya atakuwa
mgombea, nikasikia tena na Wassira naye kupitia kwa mtu wake wa karibu
ataniunga mkono, sasa namuomba mwenzangu naye Edward au maarufu kama Edo
naye aseme Profesa ndiyo wangu, ili kazi iishe na tuipunguzie kazi
Halmashauri Kuu,” alisema Profesa na kushangiliwa.
Awali Profesa Mwandosya aliwaeleza wanachama hao kuwa mwaka huu wa
uchaguzi ni mwaka mgumu sana kwa CCM na kuwataka wanachama kutofanya
mchezo katika kujibu mapigo ya wapinzani.
“Watatuuliza kuhusu EPA, wataendelea kutuuliza kuhusu Richmond,
watatuuliza kuhusu Escrow, kubwa zaidi watatuuliza kuhusu Vodacom ingawa
hili halizungumzwi lakini linakuja, lazima tujitayarishe.
“Sasa nani huyo ataweza kutusafisha, wananchi wakimtazama watasema
huyu atatusaidia na atajibu, kila ninakopita naambiwa na wananchi kuhusu
ufisadi na rushwa vinatuumiza."
"Kama chama lazima tukabiliane na hilo na hapa hatumzungumzii mtu
lazima kama chama tuyaeleze kwa wananchi. Nani atafanya hivyo wakubwa
wanajua,” alisema Profesa.
Akizungumzia wanaotishia kuhama chama, alisema wanajidanganya kwani
CCM ni maarufu zaidi ya mtu mmoja mmoja, akisema mtu pekee aliyewahi
kuhama na kukitikisa chama alikuwa Augustine Mrema, Waziri wa zamani wa
Mambo ya Ndani.
0 comments:
Post a Comment